06/02/2026
HUENDA HATA WEWE UNAMFUGA NYOKA MKUBWA SANA BILA KUJUA...
NI Kisa cha Nyoka mwenye njaa na mwanamke mwema ni kisa cha mfano,
Kisa kinachotuonya juu ya watu wanaotuzunguka kwa sura ya urafiki,
lakini ndani ya mioyo yao wamejificha k**a maadui tena wakubwa...
Ni kisa kinachotukumbusha kuwa si kila anayekukaribia anakupenda,
wapo wanaosubiri muda mwafaka ili wakumeze au wakumalize....
Inasimuliwa kuwa…
Siku moja, mwanamke mmoja mwema alimkuta nyoka mkubwa,akiwa na njaa kali na baridi kali,mwili wake ukiwa dhaifu na hauna nguvu...
Moyo wake ukamjaa huruma…
Akaamua kumuonea huruma yule nyoka.
Akamchukua, akampeleka nyumbani kwake,
akamuhifadhi, akampa makazi,akaanza kumlisha siku baada ya siku.
Muda ukapita…
Nyoka akakua mkubwa, akaanza kumzoea mwanamke yule...
Alikuwa akilala karibu naye,akimfuata kila mahali alipokwenda,kana kwamba ni rafiki wa kweli.
Lakini siku moja…
nyoka akaacha kula kabisa.
Mwanamke akahuzunika sana. akawa anamlisha kwa bidii,anamletea chakula kizuri,
lakini nyoka hakula hata chembe.
Wiki zikapita…
nyoka bado hakuli,
lakini bado anamfuata,
bado analala karibu naye,
bado anajizungusha mwilini mwake usiku akitaka joto.....
Mwanamke akafikiria sana akasema:
“Hakika nyoka wangu ni mgonjwa.”
Akaamua kumpeleka kwa daktari wa wanyama.
Daktari alipomuona nyoka, nyoka akijizungusha karibu na mwanamke huyo,
akamuliza:
“Je, ana dalili nyingine zaidi ya kukosa hamu ya kula?”
Mwanamke akasema:
“Hapana.Lakini bado analala karibu nami,hunifuatilia kwa macho,hujizungusha juu yangu usiku,lakini hataki kula kabisa.”
Daktari akatabasamu kwa huzuni…
kisha akasema kwa sauti nzito:
“Bint yangu, nyoka huyu si mgonjwa…
Anajiandaa kukula wewe.
Ameacha kula kwa makusudi
ili awe na nafasi tumboni mwake.
Anapojizungusha mwilini mwako usiku,
hapimi upendo…
anapima ukubwa wako
ili ajue k**a anaweza kukumeza.”
Maneno yale yakampiga mwanamke k**a radi.
Daktari akaendelea kusema kuwa: “Nyoka huyu Anakusanya nguvu,
anasubiri muda mwafaka wa kukushambulia.
Chukua tahadhari…
na ujitenge naye mara moja.”
Naam inaisha namna hiyo, ni hadithi ya kutisha…lakini ujumbe wake ni wa kweli sana.
Kila siku,
kuna watu wanaokaribia maisha yetu kwa tabasamu, kwa maneno matamu, kwa sura ya upole…
Lakini ndani yao,
wameficha chuki, wivu na nia mbaya na hao ndo wanatufanyia mambo ya hovyo mpaka mambo yetu yanakuwa magumu.
Sio kila mtu anaweza kubadilishwa kwa upendo.Sio kila roho ina tiba ya huruma.